MANCHESTER, ENGLAND
NI kiburi! Ni jeuri. David Moyes kumbe alikataa
ushauri wa kocha aliyepita wa Manchester United, Sir Alex Ferguson,
aliyemtaka aendelee kuwa na watu wake wa benchi la ufundi, lakini yeye
akawatimua na kuleta watu wake.
Hali ya Moyes ni mbaya Old Trafford baada ya timu
hiyo kupata pointi saba katika mechi sita na kocha wa zamani wa makipa
wa Manchester United chini ya utawala wa Ferguson, Eric Steele, ametia
chumvi kidonda baada ya kusema kuwa Moyes ni mbishi.
Steele alionyeshwa mlango wa kutokea na Moyes
pamoja na wasaidizi wengine wa zamani wa Ferguson, Mike Phelan na kocha
wa timu ya kwanza, Rene Meulensteen.
Badala yake, aliamua kuwaleta Chris Woods, Steve
Round na Jimmy Lumsden ambao alikuwa nao Everton huku pia akimteua beki
wa zamani wa United na Everton, Phil Neville kuwa mmoja wa wasaidizi
wake.
“Aliongea na mimi, Mick na Rene. Nilimwambia
kwamba nadhani ulikuwa uamuzi wa kishujaa. Alisikiliza ushauri wa
Ferguson, lakini akataka awe mtu mwenye uamuzi wake mwenyewe,” alisema
Steele.
Steele aliwasili Man United mwaka 2008 baada ya kufanya kazi na
Manchester City kabla ya hapo. Anasifika kwa
kumgeuza David De Gea kuwa mmoja kati ya makipa bora duniani baada ya
kuanza Ligi Kuu England hovyo.
Anasema kwamba anaheshimu uamuzi wa Moyes wa
kuachana na wao, lakini akaongeza kwamba haukuwa uamuzi mzuri kwa
maendeleo ya klabu.
“Sikutaka kuondoka. Nilijua kwamba David alikuwa
anakuja na nikawa najiuliza angekuja na nani. Simlaumu kwa
alichokifanya, nimekuwa katika soka kwa muda mrefu sana, lakini
inashangaza kidogo,” alisema.
“Umekutana na timu ambayo ilikuwa na msimu mzuri
na imeshinda ligi. David De Gea alikuwa na msimu bora. Inaleta maana
kama hautaki kuendelea kufanya kazi na watu waliokuwapo. Hata hivyo hilo
lipo nje ya uwezo wangu.”
Kipigo cha mabao 2-1 cha Man United kutoka kwa
West Brom Jumamosi katika uwanja wao wa nyumbani, Old Trafford,
kinaiacha United ikiwa na pointi saba katika nafasi ya 12 ikiwa ni
pointi nane nyuma ya vinara Arsenal.
No comments:
Post a Comment