KAMA huna taarifa, habarika sasa kwamba, mwili wa aliyekuwa mwongoza
filamu za Kibongo, marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ (41) aliyefariki
dunia Mei 30, mwaka huu kwa ajali mbaya ya gari nchini Tanzania na
kusafirishwa kwao,Kenya bado haujazikwa huku mazito yakiibuka kuhusiana
na msiba huo!
Chanzo cha ndani kimeliambia Amani kwamba, mwili huo utazikwa keshokutwa
Jumamosi kijijini kwao huko Kisumu baada ya kukaa mochwari kwa siku
kumi na nne tangu kifo.
WAOMBOLEZAJI WAENDELEA NA SHUGHULI ZAO
Katika hali ya kushangaza, utamaduni wa Kenya si kama wa Bongo, misiba
hupewa kipaumbele siku za mwishoni mwa wiki, hasa Jumamosi.
“Kwa sasa mwili upo mochwari, unasubiri kuzikwa Juni 14 (mwaka huu). Kwa
hiyo ukifika kwenye nyumba yenye msiba ambayo ipo Donholm, Phase 5
jijini Nairobi, unaweza kusema hakuna msiba.
Watu wanaendelea na shughuli zao za kila siku, kama kwenda sokoni na sehemu nyinginezo.
“Kifupi huwezi kujua kama kuna msiba. Huu ndiyo utaratibu wetu hapa Kenya, si kama huko Tanzania,” kilisema chanzo hicho.
Kikaendelea: “Ila Ijumaa ijayo, ndiyo kidogo kutaonesha kama kuna msiba
kwani mwili utachukuliwa kwa ajili ya taratibu za kuaga kisha Jumamosi
utapelekwa Kisumu, kwenye Kijiji cha Siaya ambako marehemu atazikwa.”
MONALISA, SONIA WALALA HOTELINI
Habari zaidi zinadai kuwa, baada ya kufika jijini Nairobi na mwili wa
marehemu, mtalaka wa marehemu, Yvonne-Cheryl Ngatikwa ‘Monalisa’, mtoto
wake, Sonia George Otieno na mama wa Monalisa, Suzan Lewis ‘Natasha’
walikuwa wakilala hotelini badala ya msibani.
WAREJEA BONGO KIMYAKIMYA BILA KUMZIKA TYSON
Ikazidi kuelezwa kwamba, licha ya kulala hotelini, wiki iliyopita, Mona,
mama yake na Sonia walirejea Bongo kimyakimya ili kuendelea na shughuli
nyingine za kila siku.
MKE MWINGINE AZUA BALAA
Wakati ya Monalisa yakiwa hivyo, aliyewahi kuwa mke wa marehemu, Beatrice naye amedaiwa kuzua balaa.
Habari zinadai kwamba, balaa la Beatrice lilianzia jijini Dar ambapo
inasemekana baada tu ya kifo cha Tyson, yeye alikwenda nyumbani kwa
marehemu na kuzuia kadi ya benki.
“Beatrice alikamata kadi ya benki (ATM) na kusema ana
haki nayo licha ya kwamba hadi anaaga dunia marehemu alikuwa akiishi na mwanamke mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Lucy.
“Ikatokea kutoelewana kati ya Beatrice na Lucy, Beatrice akawa na kadi
lakini hajui password, Lucy anajua. Mwishowe, Beatrice aliamua kumpa
kadi ndugu wa Tyson aitwaye Felix Owino,” kilisema chanzo hicho.
NAYE ALALA KWA NDUGU NAIROBI
Habari kuhusu Beatrice zikaendelea kudai kwamba, naye kama Monalisa,
alipofika jijini Nairobi na mwili wa marehemu alikuwa akilala kwa ndugu
zake badala ya msibani.
“Sijajua nini kilitokea msibani kwani baada ya kufika Nairobi na mwili
wa marehemu, Beatrice naye akawa analala kwa ndugu zake na si kwenye
nyumba iliyofikia msiba,” kilisema chanzo.
MONALISA AZUNGUMZA NA AMANI
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, juzi Amani lilimsaka Mona kwa njia ya
simu ili kujua anasema nini kuhusu mambo yaliyoelekezwa kwake.
KUHUSU KURUDI BONGO
“Ni kweli nimerudi na Sonia na mama. Ilibidi turudi kwa vile Sonia ana mitihani ya darasa la saba wiki ijayo,” alisema Monalisa.
Amani: “Lakini yule si baba yake? Kwa nini asimzike?”
Monalisa: “Nimeshakwambia labda kama una lingine.”
MADAI YA KULALA HOTELINI
Amani: “Kuna madai kwamba ulipokuwa msibani Kenya, wewe, mtoto na mama
yako mlikuwa mkilala hotelini badala ya msibani, ni kweli?”
Monalisa: “Ni kweli.”
Amani: “Kwa nini sasa?”
Monalisa: “Nafasi ilikuwa ndogo, kwa hiyo tulikuwa tunakwenda kulala hotelini, asubuhi tunaenda msibani.”
Amani: “Mona turudi kwenye kitendo cha kurudi Bongo. Kama Sonia ana
mitihani, kwa nini asirudi na mama yake wewe ukabaki kusubiri mazishi?”
Monalisa: “Misiba ya kule si kama huku Tanzania, kule siku za misiba ni
Jumamosi tu, siku nyingine watu wanaendelea na mambo yao. Sasa na
walivyochelewa kuzika sisi wengine huku (Tanzania) tuna kazi za watu
(nadhani tenda za filamu) inabidi kurudi ili kuzifanya.”
BEATRICE, LUCY HAWAKO HEWANI
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, juhudi za kuwatafuta Beatrice na
Lucy ziligonga mwamba baada ya simu zao kutokuwa hewani. Wote wapo
jijini Nairobi, Kenya wakisubiri kuzika keshokutwa.
KUHUSU MAREHEMU TYSON
George Tyson alifariki dunia kufuatia ajali mbaya ya gari aina ya Toyota
Noah, iliyotokea eneo la Gairo Morogoro. Marehemu na wenzake ambao
walijeruhiwa na wanatibiwa mpaka sasa, walikuwa wakitokea Dodoma kwenda
Dar.
Mungu ailaze mahali pema peponi. Amina.
No comments:
Post a Comment