Kamishna wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane alisema jana kuwa
Ofisi yake imefanya utafiti wa awali katika Kijiji cha Mgongo na kubaini
uwepo wa dhahabu hiyo.
Wamiminika
Gazeti hili lilikuwa la kwanza kuripoti uwepo wa dhahabu hiyo baada ya
maelfu ya watu kumiminika tena katika eneo la Samunge, lililokuwa
maarufu baada ya Mchungaji Ambilikile Mwasapile kutangaza kuwa na dawa
inayonywewa kwa kikombe kutibu maradhi sugu.
Habari kutoka Samunge zinasema wachimbaji wanazidi kumiminika kusaka
madini hayo yaliyogundulika kuwapo kwenye mashamba ya watu na maeneo ya
kingo za mto huko Mgongo, kijiji kilichopo jirani na kwa Mchungaji
Mwasapile, maarufu kama Babu wa Loliondo.
Diwani wa Samunge, Jackson Sandea alisema maelfu ya watu kutoka maeneo
mbalimbali nchini wamefurika katika kijiji hicho... “Hadi sasa kuna watu
zaidi ya 4,000 na bado wanaongezeka. Hii inaweza kuwa ni zaidi ya
kipindi kile cha Babu. Dhahabu hii inapatikana mtoni tu. Watu
wanakusanya michanga na kupata dhahabu, hakuna mtu ambaye anachimba.”
Alisema tofauti na maeneo mengine, dhahabu ya Samunge inaonekana ni ya
Watanzania wote kwani ipo eneo la mto ambao unamilikiwa na Serikali na
ndiyo sababu watu wanaingia kwa wingi. “Kuna wengine wanapata (dhahabu),
hata mashambani lakini mtoni ndipo inapatikana kwa wingi zaidi.”
Matokeo ya utafiti
“Ni kweli kuna dhahabu katika eneo la Mto Karabaline na kiasi kikubwa
kipo katika eneo la Mlima Rankiroga,” alisema Magayane. Mlima huo upo
jirani na Mto Karabaline ambako dhahabu ilianza kugundulika. Wachimbaji
wamekuwa wakiomba idhini ya Serikali kuchimba dhahabu katika mlima huo.
Magayane aliwataja wataalamu waliofanya utafiti huo kuwa ni Mtaalamu wa
Miamba, Fatuma Kijanda; Fundi Sanifu Mkuu, Zephelin Kalunde na Fundi
Sanifu Mwandamizi, Aloyce Mlaga.
Alisema uchunguzi zaidi unaendelea ili kujua ujazo wa dhahabu katika
eneo hilo na muda ambao uchimbaji unaweza kuchukua... “Tumepeleka baadhi
ya miamba katika ofisi za uchunguzi Dodoma na tunatarajia kupata
taarifa karibuni.”
Hata hivyo, alisema dhahabu inayopatikana kwenye Mto Karabaline inaweza
kumalizika ndani ya miaka miwili tofauti na ile ya mlimani ambayo
alidokeza kuwa itachukua muda kuisha.
No comments:
Post a Comment