Friday, 8 August 2014

‘Bunge la Katiba lisitishwe’


Mkurgenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba akizungumza na waandishi wa  habari kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba, jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mpiganiaji wa Haki za Binadamu, Ananilea Nkya. Picha na Rafael Lubava 

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimetaka Bunge Maalumu la Katiba kusitishwa mpaka pale maridhiano baina ya wajumbe yatakapopatikana vinginevyo Katiba itakayopatikana itakosa uhalali wa kisheria na kisiasa.
Kituo hicho pia kimelaani kauli za viongozi wa Bunge maalumu la Katiba na Serikali za kutaka kuzuiwa mijadala ya Katiba kufanywa nje ya Bunge hilo na vyombo vya habari.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo-Bisimba aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa jana kuwa hakuna haja ya kufanya haraka katika kupata Katiba Mpya ambayo haitakuwa na maridhiano na kwamba kulazimisha kuipata ni kutafuta machafuko.
“Tunapendekeza Bunge la Katiba kusitisha mijadala ya sura zilizosalia na kufanya kila liwezekanalo kumaliza mgogoro kati yao ili majadiliano yakiendelea kuwe na uhakika wa kufikia kupiga kura na mapendekezo mapya yawe na uhalali wa kisheria na kisiasa.
“Tuna uzoefu wa nchi nyingi zilizolazimisha masuala kama haya baadaye yakaleta mtafaruku. Watu wasiseme tu kuwa ni watu wachache waliosusia Bunge hapana… wale watu wana wafuasi wengi wanaowafuata ambao wanaweza kuleta balaa,” alisema Dk Bisimba.
Alisema wajumbe wote wanaoendelea na vikao katika Bunge Maalumu la Katiba hawana uhalali kuendelea kujadili rasimu hiyo kwa kuwa umoja unaowatambulisha kama wajumbe wa kuandaa katiba ya Tanzania ulishavunjika.
Bunge maalumu linaendelea na vikao vyake kujadili sura 15 za Rasimu ya Katiba, baada ya kumaliza sura ya kwanza na sita katika awamu ya kwanza, safari hii bila kuwa na wajumbe wa kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wajumbe wa umoja huo unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walitoka bungeni Aprili 16, mwaka huu wakipinga mwenendo baadhi ya wajumbe kujadili masuala yaliyo nje ya rasimu ya pili kama yalivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Dk Bisimba alibainisha kuwa hakuna haja ya kukata tamaa kutafuta maridhiano na kuongeza kuwa ili kupata mwafaka, wanahitajika wasuluhishi wasiofungamana na upande wowote unaokinzana.
Kuhusu kauli za kuzuia mijadala ya Katiba nje ya Bunge pamoja na kuwazuia waliokuwa wajumbe wa Katiba kutoa maoni yao, Dk Bisimba alisema hatua hiyo ikitekelezwa itakiuka misingi ya demokrasia na utawala wa sheria na kuminya uhuru wa vyombo vya habari na haki za binadamu kama zilivyobainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Alisema pendekezo lililotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta la kutaka Serikali kupiga marufuku vyombo vya habari kurusha matangazo ya mijadala ya katiba pamoja na agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi kuzuia mijadala hiyo katika mkoa wake ni kinyume cha Ibara za 18 na 21 ya Katiba iliyopo.
“Tabia hii ya kuwafunga midomo watoa habari na kuwafumba macho wananchi ili wasiweze kushiriki kikamilifu katika kuandika Katiba yao, haikubaliki kamwe na ni kinyume cha misingi ya demokrasia,” alisema Dk Bisimba.

No comments:

Post a Comment