KOCHA
Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mart Nooij
amefanya mabadiliko madogo katika kikosi chake kitakachomenyana na
Msumbiji, Mambas jioni ya leo Uwanja wa Zimpeto mjini hapa.
Nooij
aliyewahi kuifundisha Msumbiji, atamuanzisha Khamis Mcha ‘Vialli’
badala ya Mrisho Ngassa na Said Mourad badala ya Oscar Joshua wakati,
wengine wote ni wale walioanza mchezo wa Dar es Salaam.
Mcha aliingia kumpokea Ngassa kipindi cha pili Dar es Salaam na akafunga mabao yote mawili katika sare ya 2-2 moja kwa penalti.
Nooij
ambaye amesema anakiamini kikosi chake kuelekea mechi ya marudiano ya
hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania
tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini
Morocco, anahitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele.
La
kama si ushindi, basi sare ya kuanzia mabao 3-3, baada ya awali
kulazimishwa sare ya 2-2 na Mambas Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam- na
kama matokeo yatakuwa 2-2 tena, mchezo utahamia kwenye mikwaju penalti
kuamua timu ya kwenda kwenye kundi lenye timu za Cape Verde, Niger na
Zambia.
Akizungumza
mjini hapa baada ya mazoezi ya jana jioni, Nooij ambaye ni raia wa
Uholanzi alisema ana imani na timu yake itacheza vizuri zaidi kuliko Dar
es Salaam kwa kuwa haitakuwa katika shinikizo la mashabiki kama
nyumbani, ambalo mara nyingi hufanya wachezaji wapoteze hali ya
kujiamini.
Wachezaji
wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wamefikia
katika hoteli ya Pestana Rovuma mjini hapa baada ya kambi siku mbili
Johannesburg, Afrika Kusini na wameonyesha hali ya kujiamini kuelekea
mchezo huo.
Washambuliaji
tegemeo wa Stars, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP
Mazembe ya DRC wamesema kwamba watajitolea kila kitu katika mchezo huo
ili kuipa matokeo mazuri timu.
“Tunapita
katika mtihani mgumu, si jambo zuri kuishia hapa katika mbio za AFCON,
ambazo kwa miaka sasa tangu kizazi kilichopita tumekuwa tukisotea
fainali zake. Tutapambana, tunaomba duwa za Watanzania tu,”alisema
Samatta.
Balozi
wa Tanzania nchini hapa, Shamim Nyanduga amekuwa bega kwa bega na timu
tangu imefika hapa akisaidia maandalizi ili kuiepusha na mitego ya
hujuma za wenyeji, kuanzia chakula, usafiri hadi malazi.
Mechi
hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Uganda wakiongozwa na Dennis
Batte itaanza saa 9:00 Alasiri kwa saa za hapa, saa moja zaidi kwa saa
za nyumbani Tanzania.
Kikosi
cha Stars kinatarajiwa kuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Said Mourad, Shomary
Kapombe, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Erasto Nyoni, Thomas
Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto, John Bocco, Mbwana Samatta na Khamis Mcha
‘Vialli’.
Katika
benchi wanatarajiwa kuwapo Aishi Manula, Aggrey Morris, Oscar Joshua,
Haroun Chanongo, Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Amri Kiemba.
Wachezaji wengine waliopo hapa na timu ni Himid Mao, Shaaban Nditi na Ramadhani Singano ‘Messi’.
Katika
mechi saba zilizopita baina ya timu hizo tangu mwaka 2006, Tanzania
imeshinda moja tu, tena ya kirafiki Dar es Salaam 1-0 Novemba 19, mwaka
2008 wakati Msumbiji imeshinda mbili, moja ya kirafiki 2-0 Maputo
Novemba 19, mwaka 2008 na nyingine ya kufuzu AFCON Septemba 8, mwaka
2007 Dar es Salaam wakati mechi nne zimetoka sare.
Mholanzi
Nooij leo atakuwa anaiongoza Stars katika mechi ya saba tangu arithi
mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen, akiwa amepoteza mechi moja tu, tena ya
kirafiki 4-2 dhidi ya Botswana mjini Gaborone.
Ametoa sare tatu dhidi ya Malawi 0-0 mchezo wa kirafiki mjini Mbeya, Zimbabwe 2-2 mjini Harare kufuzu AFCON na 2-2 tena dhidi ya Msumbiji kufuzu AFCON pia mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
Ameshinda 1-0 mara mbili, dhidi ya Zimbabwe mjini Dar es Salaam kufuzu AFCON na Malawi mchezo wa kirafiki Dar es Salaam.
Kihistoria,
Tanzania imefuzu AFCON mara moja tu mwaka 1980 mjini Lagos, Nigeria,
wakati Msumbiji imecheza Fainali nne za michuano hiyo katika miaka ya
1986, 1996, 1998 na 2010, zote wakitolewa hatua ya makundi kama Taifa
Stars. Kila heri la Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
![]() |
Tuko tayari; Kocha Mart Nooij akiwaongoza vijana wake kuingia Uwanja wa Zimopeto jana tayari kwa mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo wa leo |
![]() |
Mbwana Samatta ataongoza safu ya ushambuliaji leo |
![]() |
Khamis Mcha 'Viallia' ataaza leo badala ya Mrisho Ngassa |
No comments:
Post a Comment