Tuesday, 26 August 2014

Wanajeshi wa Urusi walikuwa Ukraine kimakosa


Baadhi ya watu kumi waliokamatwa na jeshi la Ukraine
Urusi imesema kwamba kikundi cha wanajeshi wa Urusi ambacho kimekamatwa mashariki mwa Ukraine kilikuwa kimevuka mpaka huo kimakosa huku Ukraine ikisema kwamba wanajeshi 10 walikuwa wamekamatwa.

Utawala wa Kiev umetoa mahojiano ya video ya wanaume kadhaa na mmoja wao ananukuliwa akisema hivyo si vita vyao.
Tukio hilo linawadia kabla ya mkutano maalum kati ya marais wa Ukraine na Urusi ,Petro Poroshenkon na Vladimir Putin walioko mjini Minsk,Belarus.
Mapigano yanaendelea Mashariki mwa Ukraine.
Mtu mmoja katika wizara ya Ulinzi ya Urusi alinukuliwa na Shirika la habari la Urusi linalojulikana kama RIA Novosti akisema kwamba wanajeshi hao walishiriki katika doria ya sehemu ya mpaka wa Urusi na Ukraine lakini walivuka mpaka huo kimakosa katika eneo moja ambalo halina alama yoyote na kama wanavyojua, wanajeshi hao hawakuonyesha upinzani wowote kwa wanajeshi wa Ukraine walipotiwa nguvuni.
Aliendelea kwa kusema kwamba watumishi wa jeshi la Ukraine walikuwa wamepita mpaka mara kadhaa lakini hawakutilia maanani kutangaza mbali waliwarudisha waliotaka kurudi Ukraine mahali palipo salama.
Msemaji wa jeshi la Ukraine Andriy Lysenko alisema kwamba hiyo haikuwa kosa mbali na kazi ya kipekee waliyokuwa wakitekeleza.
Mwanamume mmoja anayejulikana kama Ivan Milchakov anaeleza kwamba yeye huwa kwenye mji wa Kostroma nchini Urusi na anasema kwamba hakuona walipopita mpaka.
Rais wa Urusi na mwenzake wa Ukraine wanakutana leo.
Urusi imeendelea kukataa shutuma za magharibi na Ukraine kwamba inawaunga mkono waasi hao.
Hapo jana , vyombo vya usalama vya Ukraine vilisema wanajeshi hao wa Urusi walikamatwa wakiwa kilomita 20 kutoka mpakani ndani ya Ukraine karibu na kijiji kilichoko eneo linalodhibitiwa na waasi la Donetsk.
Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko anatarajiwa kukutana na rais wa Urusi Vladimir Putin ikiwa ni mara ya kwanza tangu Juni, pamoja na maafisa wengine wa Umoja wa Ulaya katika mji mkuu wa Belarus, Minsk hii leo kujaribu kuutatua mzozo baina yao uliosababisha mapigano mashariki mwa Ukraine.

No comments:

Post a Comment