KIKOSI
cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilipata msukosuko
angani kwenye ndege kikitokea Afrika Kusini baada ya ndege ya shirika la
nchi hiyo kugeuza kurudi Johannersburg baada ya rubani kubaini
hitilafu.
Stars
iliarajiwa kufika Maputo, Msumbiji Saa 8:40 mchana kwa saa za hapa,
lakini wakiwa nusu ya safari walitangaziwa kutokea matatizo ambayo
yaliifanya irejee Uwanja wa Ndege wa O R Tambo kwa matengenezo.
Baada
ya matengenezo ya takriban saa moja, ndege hiyo ilipaa tena na kufika
Maputo Saa 11:30 za huku, tayari kwa mchezo wa marudiano hatua ya mwisho
ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza
Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco.
Katika
mchezo huo utakaofanyika Jumapili, Stars inahitaji ushindi wa ugenini
au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga mbele, baada ya awali
kulazimishwa sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ofisa
Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface
Wambura amesema begi la jezi ambazo zitatumika kwenye mchezo wa Jumapili
limesahaulika Johannesburg na tayari wametoa taarifa kwa wahusika,
Shirika la ndege la Afrika Kusini ili liletwe kesho.
Wachezaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu watawasili kesho asubuhi wakitokea Afrika Kusini.
Baada
ya kuwasili, kocha Mkuu wa Stars, Mart Nooij raia wa Uholanzi
aliwaambia Waandishi wa Habari kwamba wachezaji wake wote wako fiti
kuelekea mchezo wa Jumapili na wenyeji Mambas.
Amesema
hana majeruhi hata mmoja kikosini mwake na kambi yao ya siku mbili
nchini Afrika Kusini ilikuwa nzuri na amewataka Watanzania wawe na imani
na timu yao kuelekea mchezo huo.
Hata
hivyo, Nooij alisema wachezaji wake walipata hofu baada ya hitilafu
zilizotokea kwenye ndege, lakini imechangia pia kuwajenga kisaikolojia.
Nooij
alipokewa vizuri na raia wa Msumbiji kuanzia wafanyakazi wa Uwanja wa
ndege wa Kimataifa wa Maputo kutokana na kukumbuka kazi yake nzuri
alipokuwa kocha wa Mambas kabla ya kwenda Ethiopia na baadaye Tanzania.
Kiungo
mwandamizi wa timu hiyo, Amri Kiemba amesema wamekuja Msumbiji kwa
ajili ya kitu kimoja tu, kuhakikisha wanashinda na kusonga mbele.
Beki
Aggrey Morris ambaye anaweza kuanza Jumapili badala ya Kevin Yondan,
amesema; “Kambi ya Afrika Kusini ilikuwa nzuri, tulifanya mazoezi mazuri
na wachezaji wako fiti na wana ari ya ushindi,”.
Kwa ujumla wachezaji wa Stars wamewasili wakiwa vizuri jioni ya leo pamoja na misukosuko waliyoipata njiani.
Katika
mchezo wa kwanza, Dar es Salaam mabao ya Stars yalifungwa na kiungo wa
Azam FC, Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyeingia kipindi cha pili kuchukua
nafasi ya Mrisho Ngassa.
Dakika
45 za kwanza zilimalizika bila bao na kipindi cha pili, Msumbiji
walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 47 kwa penalti iliyokwamishwa
nyavuni na Elias Pelembe baada ya Kevin Yondan kumcheza rafu kwenye eneo
la hatari. Mcha aliisawazishia Stars bao hilo dakika ya 65 akimalizia
krosi nzuri ya Thomas Ulimwengu.
Mcha
tena akaifungia Stars bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 71 kwa
penalti, baada ya mabeki wa Mambas kumchezea rafu Mbwana Samatta kwenye
eneo la hatari.
Stars
iliongeza mashambulizi langoni mwa Msumbiji na kukosa mabao kadhaa ya
wazi. Msumbiji walizinduka na kufanya shambulizi zuri lililowapatia bao
la kusawazisha dakika ya 87 kupitia kwa Isaac Carvalho aliyetokea benchi
pia.
Stars
sasa itajitaji ushindi wa ugenini ili kusonga mbele, au sare ya kuanzia
mabao 3-3, wakati wenyeji wanaweza kunufaika na sare ya 1-1 au 0-0.
Ikiwa 2-2 tena, mshindi ataamuliwa kwa mikwaju ya penalti.
Stars
iliyofika hatua hii baada ya kuitoa Zimbabwe kwa jumla ya mabao 3-2
ikishinda 1-0 nyumbani na sare ya 2-2 Harare, ikifanikiwa kuitoa
Msumbiji itapangwa katika Kundi C ambalo lina timu za Zambia, Cerpe
Verde na Niger zilizofuzu moja kwa moja hatua hiyo, kuwania tiketi ya
Morocco mwakani.
![]() |
Kocha wa Stars, Mart Nooij kushoto akizungumza na Waandishi wa Habari |
![]() |
Beki wa Stars, Aggrey Morris akiwasili Maputo |
![]() |
Kutoka kulia Haroun Chanongo, Simon Msuva na Mrisho Ngassa |
![]() |
Mwinyi Kazimoto kwenye basi kuelekea hotelini Maputo |
No comments:
Post a Comment