Monday, 12 May 2014

DALALI AMPA MAAGIZO MAZITO AVEVA NA MPIRA JUU

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Hassan Daalal amemtaka mgombea Urais wa klabu hiyo, Evans Aveva avunje makundi saba yanayoigawa klabu hiyo kwa sasa, iwapo atafanikiwa kuingia madarakani.  Ameyataja makundi hayo kuwa ni Simba Ushindi, Robialac Friends, Simba Chai, Simba Futari, Tia Mchuzi Kwangu Pakavu na Simba Poa ambayo ni ile inayofurahi hata timu yao ikifungwa. Daalal leo amemsindikiza Aveva kurejesha fomu ambayo aliichukua jana kuwania cheo hicho katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.
Daalal akimsindikiza Aveva kurejesha fomu leo
Dalali amesema kuwa alikuwa na nia ya kuwania cheo hicho lakini baada ya kuona Aveva amechukua fomu aliamua kuacha dhamira yake na kuwataka wanachama wa Simba kumchagua mgombea huyo kwa sababu ni mtu mwadilifu, mwaminifu, mwenye upendo na asiye na ubaguzi. Alisema kwamba anaamini Aveva akichaguliwa atahakikisha anamaliza makundi yaliyopo ndani ya klabu yao, ataleta umoja na kuendeleza mazuri ya ndani ya uwanja ambayo ni kupata pointi tatu. "Nilipoondoka mwaka 2010 niliondoka na mpira wangu, sasa nakukabidhi ili uhakikishe pointi tatu zinapatikana, na ninaamini atawarudisha wazee ambao miaka minne iliyopita walifukuzwa, nyumba bila ya wazee haiendi," alisema Dalali. Katibu Msaidizi wa Kamati ya Uchaguzi, Khalid Kamguna, alisema kuwa bado anatoa wito kwa wagombea kujitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hizo saba zilizotangazwa ili waweze kuitumikia klabu hiyo. Kamguna aliwataja wagombea wengine ambao walichukua fomu jana mbali ya Wambura kuwa ni pamoja na Meddy Milanzi, Collin Frisch, Chano Hassan, Khamis Mkoma, Salim Jazaa, Emmanuel Kazimoto, Juma Abbas (Pinto) na Amina Poyo ambaye ndiye mwanamke pekee ambaye amejitokeza katika uchaguzi huo nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji. Aliwataja wagombea waliorejea kuwa ni Iddi Kajuna, Ramson Rutiginga, Said Tully, Suleiman Dewji wanaowania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na Andrew Tupa anayegombea cheo cha Urais wa Simba. Alisema kuwa mwisho wa zoezi hilo la kuchukua na kurejesha fomu ni kesho Jumatano saa 10 kamili jioni.

No comments:

Post a Comment