MCHEZO wa kwanza wa mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya
kuwaka tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika Morocco 2015 baina ya wenyeji
Tanzania dhidi ya Zimbabwe unaweza kufanyika mjini Mbeya, Mei 18, mwaka huu,
imefahamika.
Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati
(CECAFA), Nicholas Musonye jana alikuwa mjini Mbeya kuukagua Uwanja wa Sokoine
kama unakidhi sifa za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) za mechi za kimataifa na
inasemekana ripoti yake ni nzuri.
Tanzania, au Taifa Stars ilicheza mchezo wa kirafiki na Malawi
kwenye Uwanja huo Mei 4, mwaka huu na kwa namna ambavyo mashabiki wa soka mjini
Mbeya waliisapoti timu yao ya taifa, Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF),
Jamal Malinzi alitamani timu hiyo icheze tena kwenye Uwanja huo.
Na kutokana na mechi za Stars hivi sasa kukosa mvuto Dar es Salaam
kwa sababu ya matokeo mabaya, hata wachezaji wamependa kucheza mechi zao
mikoani na Mbeya wameona panafaa kuanzia.
Wakati wowote kuanzia sasa TFF inatarajiwa kutoa tamko rasmi
kuhusu mchezo huo kwamba utafanyika Mbeya, au sehemu nyingine.
Tanzania ikifanikiwa kuitoa Zimbabwe itamenyana na mshindi baina ya
Msumbiji na Sudan Kusini kuwania kuingia katika hatua ya makundi.
Na ikifuzu hapo itaingizwa Kundi F pamoja na Zambia, Cerpe Verde na Niger kuwania kwenda Morocco 2015.
No comments:
Post a Comment