WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Uratibu na Bunge, amesema, si makosa raia wa Tanzania kuhofia
majeshi ya ulinzi kuchukua nchi ikiwa muundo wa Muungano wa serikali
mbili ukibadilishwa na kuwa serikali tatu.
Aidha, amesema pia ana hofu kuhusu
mwenendo wa CUF unaoshirikiana kisiasa na Taasisi ya kidini ya Uamsho,
inayotekeleza majukumu yake Zanzibar kwamba umelenga kuua Muungano na
kuhatarisha amani kwa mgongo wa dini ya Kiislamu.
Lukuvi alisema hayo bungeni, alipotoa
ufafanuzi wa kauli zake alizozitoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la
Dodoma wakati wa Ibada ya kumsimika Mchungaji Joseph Bundala kuwa Askofu
wa Kanisa hilo.
Kauli hiyo ndio iliyodaiwa na Ukawa kuwa moja ya sababu ya kutoka nje ya Bunge kususia kikao.
Madai mengine ya Ukawa yalikuwa ni
ubaguzi, matusi na vitisho vinavyoendelea bungeni. Katika ufafanuzi wake
Lukuvi alisema kwamba mfumo wa serikali tatu unaweza ukasababisha nchi
kupinduliwa na Jeshi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaweza
ikaongozwa na CUF kwa Sera za Kikundi cha Uamsho jambo linalompa hofu ya
udini na kuvunjika kwa amani.
Lukuvi ambaye jana alilazimika kukatisha
safari yake ya kwenda India kwa matibabu, alisema alichoeleza katika
hafla hiyo ya kumsimika Askofu ni hofu zake binafsi kuhusu muundo wa
serikali tatu.
“Wote nikiwauliza hapa uamsho ni nani
mtasema ni CUF, kwa nini sasa nisiwe na hofu ya kidini wakati kuna chama
cha siasa ambacho kinamiliki taasisi inaitwa Uamsho lakini ina ladha ya
kidini, hizo ndizo sera zao, unakuwaje na chama cha siasa
kinachojipanga kutawala Zanzibar lakini kinaendeshwa na sera za Uamsho?
“Wanachosema CUF ndicho wanachosema
Uamsho, wakisema serikali tatu ngangari, wakisema serikali ya mkataba
sawa kabisa, wapi umeona vikundi kama hivyo, ukiona chama
kinajitayarisha kuchukua madaraka na kinatumia taasisi hii kueneza sera
zake ni hatari kwa mustakabali wa nchi,” alisema.
Akizungumzia hofu ya nchi kupinduliwa,
Lukuvi alisema katika muundo wa Serikali tatu, Rais wa shirikisho hawezi
kuwa Amiri Jeshi Mkuu, kutokana na kutokuwa na vyanzo vya mapato hivyo
haiwezi kuendesha vyombo vya dola kama Jeshi na Polisi ambao mara nyingi
bajeti zao ni kubwa na hazijawahi kutosha hata katika serikali mbili za
sasa.
“Kwa mfumo huu wa serikali tatu,
tusiwatafutie sababu wanajeshi wetu, mimi nilishasema sitashiriki
kutafuta vyanzo kwa serikali ya tatu badala yake naukataa muundo huu,”
alisema Lukuvi na kuongeza kuwa katika ukosefu mkubwa wa mapato, majeshi
yahawezi kuvumilia lazima kutokee uasi na hiyo ndio hofu yake.
No comments:
Post a Comment