Friday, 11 April 2014

BIASHARA ZA FIGO YASHAMIRI NCHINI..ZAUZWA KAMA

Katika kile kinachoonekana kukithiri kwa hali
ngumu ya maisha, baadhi ya Watanzania
wameanza biashara ya kuuza figo zao kwa
gharama kubwa kwa watu wenye mahitaji ya
kiungo hicho muhimu mwilini.
Uuzaji huo umetokana na ongezeko la maradhi
ya figo miongoni mwa Watanzania kwani
takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
zinaeleza kuwa kuna wagonjwa 470,000 nchini
ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi
kabisa na wanahitaji upandikizaji. Katika
uchunguzi wake, mwandishi wa gazeti hili
alifanya kazi ya kutafuta kama wafanyavyo watu
wengine wenye mahitaji hayo na alifanikiwa
kukutana na watu kadhaa ambao walikuwa
tayari kumwuzia lakini kwa gharama kubwa.
Kijana mmoja alikuwa tayari kumwuzia figo
mwandishi wetu. Katika kufikia makubaliano
mazungumzo ya kijana huyo, Abiyudi Mtaki na
mwandishi wetu yalikuwa hivi:
Mwandishi: “Habari yako kaka, nimepata namba
yako kutoka kwa (jina linahifadhiwa) amesema
upo tayari kuuza figo yako, mimi nina shida kwa
sababu mama yangu anahitaji na hali yake si
nzuri.”
Muuzaji: “Nitumie meseji nipo kwenye gari.”
Alipotumiwa meseji alijibu hivi: “Dada yangu
mimi naelekea Uganda, kuna mtu kanitumia tiketi
jana, wakala nilimwambia kuwa nauza, ila yeye
hakuniambia iwapo kuna mtu wa Dar es Salaam
anayehitaji.”
Mwandishi: “Jamani kaka tusaidie kwa sababu
tuna shida, kwani huyo wa Uganda anakupa
shilingi ngapi?”
Muuzaji: “Napata milioni 80 aisee!”
Mwandishi: “Basi sitaweza kupata hizo fedha,
ngoja niangalie namna nyingine.”
Muuzaji: “Kwani we ulikuwa na ngapi?”
Mwandishi: “Tuna shilingi milioni 20 tu.”
Kiwango hicho hakikukubaliwa na muuzaji huyo.
Mei mwaka jana, Mwanahabari wa Gazeti la The
Telegraph la Uingereza alituma ujumbe kwenye
ukurasa wake wa facebook na kujifanya kuwa ni
kaka wa mwanamke anayehitaji kupandikizwa
figo hivyo anahitaji mtu anayeuza.
Ndani ya wiki moja alipata wateja zaidi ya 16
kutoka Uingereza, India na Tanzania waliojitolea
kuuza figo zao kwa gharama ya Euro 20,000
hadi 30,000, zaidi ya Sh68 milioni. Daktari
Bingwa wa figo kutoka Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Linda Ezekiel alisema uuzaji wa
figo ni kosa la jinai kwani kisheria ni makosa
kuuza kiungo cha binadamu kwa gharama
yoyote.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Figo Tanzania, Jaji
Frederick Werema alishangazwa na hatua za
baadhi ya watu kuchukua uamuzi wa kuuza figo
kwa ajili ya kujipatia fedha.
“Kutoa figo ni kosa la jinai, lakini si hivyo tu,
kutoa figo ni lazima ufuate taratibu za kisheria
na za kitabibu,” alisema Jaji Werema, ambaye
pia ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja
alisema miongozo na sera za Wizara ya Afya
hazikubaliani na biashara ya uuzaji wa figo
kama ilivyo kwa uuzaji wa damu.

No comments:

Post a Comment