KWAKO Elizabeth Michael ‘Lulu’. Leo nimeona
nikukumbuke kupitia barua! Natambua uwezo
wako mkubwa katika kazi, juhudi zako binafsi
ndiyo zimekufikisha hapo ulipo, mataifa
mbalimbali sasa wanatambua kuwa kuna mtu
anaitwa Lulu, yupo Bongo, muigizaji!.
Sitaki kukurudisha sana nyuma lakini najua
unajua kuwa ni jinsi gani kipindi cha nyuma
ulikuwa ukipamba vyombo vya habari kwa
skendo chafu. Ulipoteza dira ya kimaisha, watu
wengi waliokuwa wakikufuatilia kazi zako
walianza kukutupa.
Walikupotezea kwa sababu ya matukio ya ulevi,
mavazi ya nusu utupu na matukio mengi ya
ajabuajabu yaliyofanana na hayo. Sina nia
mbaya kukumbusha lakini waswahili wanasema
binadamu anajifunza kutokana na makosa.
Maishani mwako umekutana na mazito
yasiyofanana na umri wako.
Kwenye ulimwengu wa mahaba, ilikuwepo
minong’ono mingi juu ya watu wanaotajwa
kushiriki mapenzi na wewe, walitajwa vigogo,
mastaa na hata wasio mastaa. Sitaki kusema ni
kweli au la lakini lisemwalo kama halipo, ujue
laja.
Siri ilifichuka kupitia kifo cha yule unayedai
alikuwa mwandani wako, marehemu Steven
Kanumba.
Mazingira ya kifo chake, umri mdogo uliokuwa
nao ilikuwa ni fundisho kubwa maishani mwako.
Ulipambana na msalaba wa gereza, ukapambana
na mlolongo wa kesi mahakamani hadi pale
ulipofanikiwa kutoka kwa dhamana, Januari
mwaka jana.
Baada ya kutoka mahabusu, kwa kipindi cha
takriban mwaka mmoja sasa ulikuwa kimya,
ulionekana kubadilika kitabia. Yale uliyokuwa
ukiyafanya awali, uliyaweka pembeni na zaidi
kusimamia mustakabali mzima wa maisha yako,
ulikuwa mwema sana aisee!.
Kinachonisikitisha ni kuanza kusikia tena matukio
ya ajabu, unaonekana kubadilika. Nimefuatilia
tabia zako, naona umeanza kubadilika,
umesahau eeeh! Mavazi yako kwa miezi
michache iliyopita, nimegundua yanaanza
kuchepuka! Mfano mzuri ni kigauni ulichokivaa
mwishoni mwa wiki iliyopita katika sherehe yako
ya kuzaliwa.
Hakikustiri maungo yako nyeti, kilionesha
sehemu kubwa ya matiti yako.
Kama hiyo haitoshi, kupitia mitandao ya kijamii
umeanza kushusha matusi mazito bila sababu
za msingi, mtu akikukosoa kidogo, unampa
maneno machafu ambayo hayaandikiki gazetini.
Kama kioo cha jamii, unapaswa kuvumilia mengi.
Nikiwa kwenye kazi zangu za kila siku, huwa
nakuwa wa kwanza kupata fununu za
mabadiliko ya kila msanii na namna anavyoishi.
Nikuonye tu, kuwa makini na mwenendo wako
kwani tayari jamii ilishaanza kujenga imani na
wewe. Uliaminika na ndiyo maana ukapata
bahati ya kuchukuliwa katika kampuni nzuri
ikakusimamia kazi zako hadi sasa.
Kwa kuwa tayari nimeanza kupata malalamiko
kutoka katika vyanzo vyangu, nikusihi sana
mdogo wangu, usirudi ulipotoka. Jenga heshima
mpya na jamii ikuamini kutokana na kazi zako
na si skendo za ajabuajabu, kwa leo ni hayo tu!
Wasalam.
Wednesday, 23 April 2014
HII NDIO BARUA NZITO KUTOKA GPL KWENDA KWA LULU, UNAWEZA ISOMA HAPA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment