Tuesday, 15 April 2014

JAMAL MALINZI AGOMA KUJIUZULU UENYEKITI WAKE

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),
Jamal Malinzi amesema hatajiuzulu nafasi ya
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa
Kagera (KRFA) pamoja na kuwa na majukumu ya
kitaifa.
Katika taarifa yake aliyoitoa mbele ya wajumbe
wa mkutano mkuu wa KRFA mkoani hapa juzi
Jumamosi, Malinzi alisema wakati anakuja
kuhudhuria mkutano huo alikuwa na wazo la
kujiuzulu.
Hata hivyo aliwaeleza wajumbe hao kuwa
ameachana na wazo la kujiuzulu nafasi ya
uenyekiti wa KRFA, kwa kuwa aliombwa na
wajumbe asichukue hatua hiyo.
Alisema baadhi ya wajumbe wa KRFA walitishia
kuachia nafasi zao endapo angejiuzulu nafasi
yake ndani ya chama hicho ili aendelee
kutumikia nafasi moja ya Rais wa TFF.
Pia alisema ameamua kuendelea ili kuzima
uvumi kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka
waliodai kuwa aligombea nafasi ya uenyekiti wa
KRFA ili apate tiketi ya kugombea kiti cha urais
wa TFF.
Katika hotuba yake kwa wajumbe hao Malinzi
aliwataka kuhakikisha wanashirikiana na
halmashauri za wilaya ili kutenga maeneo ya
viwanja vya michezo na kusema Uwanja wa
Kaitaba utawekewa nyasi bandia baada ya
kupata ufadhili wa Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa).

No comments:

Post a Comment