Saturday, 19 April 2014

JERR SILAA" YANGA HAKUNA KUJENGA UWANJA JAGWANI ..PALE NI MKONDO WA MAJI"

Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa
amepigilia msumari wa mwisho kwa kuwataka
Yanga kusahau kuhusu ongezeko la eneo la
kujenga uwanja wake eneo la Jangwani kwa vile
sehemu hiyo ni mkondo wa maji.
Akizungumza na gazeti hili, Dar es Salaam jana,
Silaa alisema:
“Tumepata hasara kubwa (Serikali) hii yote
imetokana na watu kujimegea maeneo na
kujenga kwenye mkondo wa maji, mafuriko yote
haya yanayotokea ni kwa vile maji yanakosa pa
kwenda na kuishia kwenye maeneo mengine
ndiyo maafa yote haya yanatokea.
“Hebu angalieni pale Jangwani sasa hivi kulivyo,
maji yamefurika watu wengine wamepoteza
maisha, halafu bado turuhusu watu waendelee
kujenga kwenye mkondo wa bahari, waambieni
wasahau hilo.”
Kauli hiyo ya Meya Silaa imekuja siku chache
baada ya Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC)
kudai kuwa eneo ambalo wanaliomba Yanga ni
hatarishi, hivyo watafute eneo lingine kwa ajili ya
ujenzi wa uwanja wao kama kweli uongozi uliopo
chini ya Mwenyekiti wake, Yusuf Manji, una nia
ya kuwajengea Wanayanga uwanja.
Eneo hilo la Jangwani, mbali ya kuwa ni bonde
kubwa la Mto Msimbazi, ambalo ni mkondo wa
upumuaji wa bahari, lakini pia kuna bomba
kubwa linalopeleka maji Hospitali ya Taifa
Muhimbili na lingine linalopeleka maji taka
baharini.
Hata hivyo, licha ya Yanga kushauri kuondoka
eneo hilo ambalo ni hatarishi, uongozi wa klabu
hiyo chini ya Mwenyekiti wake wa
Ujenzi wa Uwanja, Francis Kifukwe, umezidi
kusisitiza kuwa kuna masharti ambayo NEMC
wamewapa na wakiyatimiza eneo hilo watapewa
ikiwemo kubeba fidia za kuwalipa wakazi wa
eneo hilo.
“Kuna masharti ambayo wametupa na sisi tupo
tayari kuyatekeleza hawajatuambia chochote,
huyo aliyekwambia tumenyimwa kujenga uwanja
ni nani? Nitajie huyo mtu wa NEMC,
ninachoweza kusema kuna masharti na
maelekezo ambayo wametupa,” alisema Kifukwe
huku akigoma kuzungumzia suala hilo kwa
undani kwa kueleza masharti na mapendekezo
waliyopewa.
Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya
Manispaa ya Ilala ilikutana hivi karibuni kujadili
suala hilo ambalo hata hivyo wameliacha
mikononi mwa NEMC.
Nayo Kamati ya Mipango Miji na Mazingira ya
Manispaa ya Ilala ilifanya ziara ya ukaguzi wa
Jangwani hivi karibuni
Wakati huohuo; Mvua hizo zinazoendelea
kunyesha zimesababisha ukuta mkubwa wa uzio
wa uwanja wa Yanga, ambao umejaa maji kwa
sasa kubomoka. Ukuta huo ni ule ambao upo
upande wa bonde la Msimbazi chini ya uwanja
huo.

No comments:

Post a Comment