Thursday, 24 April 2014

HAYA NDIO MASWALI 7 YA JAJI WALIOBA KWA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA..

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
ameuliza maswali saba ya msingi kwa
wajumbe wa Bunge la Katiba wanaopinga
Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume yake
akitaka wawajibu wananchi ili kutuliza kiu
yao.
Jaji Warioba ambaye tangu awasilishe
Rasimu ya Katiba Desemba 30, mwaka
jana amegeuka kuwa adui kwa watu
wanaotaka muundo wa serikali mbili,
aliuliza maswali hayo jana katika uzinduzi
wa ripoti ya utafiti wa Taasisi ya Twaweza
kuhusu mchakato wa Katiba.
Akizungumza kwa ukali, Jaji Warioba
alisema: "Kwanza, jibuni kwa nini
mnapinga muundo wa Muungano wakati
walioupendekeza ni wananchi?
"Sheria inasema uwepo wa Muungano na
mapendekezo katika rasimu hayasemi
Muungano usiwepo. Kumbukeni kuwa
wananchi walitakiwa kutoa mapendekezo
ya namna ya kuboresha Muungano."
Katika swali lake la pili, Warioba alisema
kwa nini Tanganyika imevaa koti la
Muungano? Kwa kuwa katika ukusanyaji
wa maoni wananchi walieleza kuwa Serikali
ya Muungano ya sasa siyo ya Muungano,
ni ya Tanganyika.
Katika swali la tatu alisema wajumbe hao
wanatakiwa kujibu maelezo ya wananchi
ambao waliieleza tume hiyo kuwa Katiba
imevunjwa na madaraka ya rais
yamechukuliwa na sasa kuna marais
wawili katika nchi moja.
"Tume inapewa lawama kubwa, wajibuni
wananchi hii tume ilitumwa na nani
kukusanya maoni ya wananchi? Waambieni
ilikusanya maoni hayo kwa kutumia sheria
ipi zaidi ya ile ya Mabadiliko ya Katiba?"
alisema Jaji Warioba katika swali lake la
nne.
Katika swali lake la tano, Warioba aliwataka
wajumbe hao kutoa sababu za kumtuhumu
kuwa amependekeza muundo wa serikali
tatu kwa sababu yeye pamoja na (Joseph
Butiku) walikuwa wajumbe wa Tume ya Jaji
Kisanga na Jaji Nyalali ambazo nazo
zilipendekeza muundo wa serikali tatu, kitu
ambacho alisema si kweli na hawakuwahi
kuwa mjumbe wa tume hizo.
Pia, aliwataka wajumbe hao kujibu swali la
sita, kwa nini hawataki kuzungumzia
yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na
badala yake wanageuza rasimu hiyo kuwa
imeandikwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Katika swali lake la saba, aliwataka
wajumbe kujibu kwa nini wanaishutumu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa
imeingiza maoni yake, wakati ilikusanya
maoni hayo kwa mujibu wa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba?
Alisema badala ya kujadili hoja za msingi,
wajumbe wa Bunge hilo wamekuwa wakitoa
lugha za kejeli na matusi kwa baadhi ya
watu (akiwamo na yeye), kitendo ambacho
alisema si sahihi na kinaweza kuligawa
taifa kwa sababu yaliyomo katika Rasimu
ya Katiba yametokana na maoni ya
wananchi.
Katika uzinduzi huo walikuwepo baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo ambao ni Dk
Hamisi Kigwangalla aliyemwakilisha Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Julius
Mtatiro, Maria Sarungi na aliyekuwa
mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Humphrey Polepole.

No comments:

Post a Comment